Majibu ya NEC kuhusu waandishi wa habari kwenye vituo vya kupiga kura.

Mkurugenzi wa Nec, Ramadhani Kailima

Kwa mara ya kwanza Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) imeruhusu waandishi wa habari kufika kwenye vituo vya kupigia kura na kufanya mahojiano na wapiga kura pamoja na wasimamizi wa uchaguzi wakati wa upigaji kura uchaguzi mkuu Oktoba 25, mwaka huu.
Mkurugenzi wa Nec, Ramadhani Kailima, alisema hayo wakati wa mafunzo ya siku mbili ya waratibu wa uchaguzi, wasimamizi wa uchaguzi ngazi ya majimbo na wilaya na maafisa wa uchaguzi yaliyofanyika mjini hapa.
“Uchaguzi wa mwaka huu ni wa kihistoria, kwa mara ya kwanza waandishi wa habari wataruhusiwa kufika katika vituo vya uchaguzi kwa ajili ya kupata habari kutoka kwa wasimamizi wa uchuguzi na hata wapiga kura kuhusu namna  uchaguzi huo utakaofanyika,” alisema.  Hata hivyo, Kailima alisema katika kufanikisha hilo, tume inaandaa mwongozo utakaoeleza taratibu na mipaka ya waandishi wa habari pamoja na watakaohusika kutoa habari katika vituo hivyo vya kupigia kura.
UTABIRI WA MVUA
Katika hatua nyingine, Kailima alisema Nec imepata taarifa kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inayotabiri kuwa Oktoba kutakuwa na mvua, hivyo tume hiyo imejiandaa kukabiliana na changamoto hiyo.
Hivyo aliwataka wasimamizi wa uchaguzi kubaini mapema maeneo ambayo yanaweza kuingia maji na kuweka tahadhari ili kuepuka usumbufu kwa wapigakura ama uharibifu wa vifaa vya kupigia kura zikiwamo karatasi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Rajabu Rutengwe, aliwataka wasimamizi wa uchaguzi wawe makini katika kutekeleza majukumu yao ili mchakato wa uchaguzi ufanyike kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizopo, kinyume cha hayo wanaweza kusababisha kutoaminika.  
Dk. Rutengwe pia aliwataka viongozi wa vyama vya siasa kuwaelimisha na kuwahamasisha wananchi kujitokeza kupiga kura badala ya kuchochea vurugu, kwani amani ikitoweka kuirudisha ni gharama kubwa.
CHANZO: NIPASHE
Share on Google Plus

About Unknown

0 comments:

Post a Comment