Mgombea urais wa ACT Wazalendo aahidi mema Lindi.


Mgombea urais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania kupitia chama cha ACT Wazalendo Anna Mghwira amewaahidi wananchi wa mkoa wa Lindi kuboresha miundombinu ya barabara na kujenga kiwanda cha korosho ili kurahisisha mawasiliano kati ya wilaya hizo na mkoa ikiwa atachaguliwa kuwa rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania.
Anna Mghwira ametoa ahadi hiyo wilayani Liwale wakati akiwahutubia wananchi katika mkutano wa kampeni za kuomba kuchaguliwa ambapo amesema pamoja na azma hiyo ataongeza ukusanyaji wa kodi ili kukidhi mahitaji ya huduma za jamii na kupunguza misamaha ya kodi.
Mapema mgombea huyo wa urais akiwa njiani kuelekea Liwale alizuiwa na wananchi waliokuwa wamefunga barabara katika wilaya ya Nachingwea wakimtaka awahutubie ambapo alilazika kuwahutubia na kueleza azma yake ya kuunda serikali yenye uadilifu, utu na uzalendo.
Kwa upande wao wagombea ubunge katika majimbo ya Nachingwea na Liwale walimweleza mgombea huyo kuwamajimbo yao na mkoa wa Lindi kwa ujumla unakabiliwa na matatizo ya ukosefu wa huduma bora za afya, miundombinu duni ya barabara, maji, elimu, soko la korosho na unyanyasaji na mauaji katika hifadhi ya msitu wa Serou


SOURCE: ITV TANZANIA
Share on Google Plus

About Aldo Simon

0 comments:

Post a Comment