Katibu wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi Mukajanga
Dar es Salaam. Kwa mara nyingine, magazeti ya Mwananchi yameibuka kinara kwa kuandika habari za uchaguzi bila upendeleo, kwa kuzingatia weledi na kuwapa wananchi nafasi ya kuzungumza na wagombea wao.
Hii ni mara ya pili kwa Mwananchi na The Citizen yanayochapishwa na kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL), kutajwa katika ripoti ya pili ya Baraza la Habari Tanzania (MCT) inayoangalia mwenendo wa uandishi wa vyombo vya habari katika Uchaguzi Mkuu.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyotolewa jana, kati ya magazeti 13 yaliyofanyiwa uchunguzi, Mwananchi na The Citizen yameongoza na kuonekana yamekuwa yakifanya bidii kuhakikisha yanaandika habari nyingi za uchaguzi pasipo upendeleo kwa chama chochote na kuzingatia hoja za kampeni badala ya vihoja.
Mbali na mengine ambayo habari zake za uchaguzi zilifuatiliwa ni Zanzibar Leo, Daily News, The Guardian, Habari Leo, Nipashe, Uhuru, Tanzania Daima, Mtanzania, Rai Tanzania, Jambo Leo, na Majira.
Ripoti hiyo ilionyesha kuwa, katika kipindi cha kuelekea Oktoba 25, ambayo ni siku ya kupiga kura, Mwananchi imekwepa kutoa habari zenye msemaji mmoja na badala yake imekuwa ikiwapa wasemaji wengi kuzungumza kwenye habari moja.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa gazeti hilo limekuwa likitoa fursa ya watuhumiwa kujibu tuhuma zao sambamba na kuandika habari zake za uchaguzi kwa kina zaidi.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa katika kipindi ambacho magazeti hayo yamechunguzwa jinsi yanavyoripoti shughuli za uchaguzi, Mwananchi iliandika habari zinazoonyesha wananchi wanasemaje na si habari ambazo zilionyesha wanayosema wagombea pekee.
Kwa upande wa The Citizen, ripoti hiyo inaonyesha kuwa gazeti hilo limekuwa likiandika habari kwa usahihi bila kupendelea huku likitoa nafasi kwa watoaji wengi wa habari.
Taarifa hiyo ilisema katika kipindi cha Septemba 11 hadi 17 mwaka huu, Mwananchi iliongoza kwa kuandika habari 98 za uchaguzi, huku The Citizen likiandika habari 66.
Ukiondoa magazeti hayo, mengine yaliyotajwa kuripoti habari nyingi za uchaguzi ni Tanzania Daima yenye 89 na Jambo Leo 79.
Taarifa hiyo ilisema kuwa baadhi ya magazeti yamekuwa yakiandika habari kwa upendeleo kwa vyama, huku yakitoa nafasi finyu kwa vyama yasiyoviunga mkono.
Katika ripoti ya Septemba 21, MCT ilisema kuwa Mwananchi imekuwa ikivipatia nafasi vyama vyote bila kujali ukubwa au udogo wake, sambamba na kuwapa wananchi nafasi ya kuzungumzia uchaguzi na kampeni.

0 comments:
Post a Comment