Kipindupindu chaingia Moro, Shinyanga, mmoja afariki


Morogoro/Shinyanga. Wakazi wa Kata ya Mindu Manispaa ya Morogoro wamekumbwa na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu ambapo hadi sasa mtu mmoja ameripotiwa kufa na hivyo kuzua hofu kwa wakazi wa eneo hilo na manispaa kwa ujumla.

Akizungumza na Mwananchi Katika Kambi maalumu ya wagonjwa wa Kipindupindu, Afisa Afya wa Manispaa ya Morogoro, Gabriel Malisa alimtaja aliyefariki kuwa ni Mkolole Shomari (65).
Amesema kuwa mtu huyo alifariki nyumbani kwake maeneo ya Mindu baada ya majirani zake ambao wametokea Dar es salam kuwa na ugonjwa huo licha ya kuwa walianza kutibiwa Amesema kuwa baada ya muda mfupi marehemu alianzwa na dalili za ugonjwa huo za kuharisha na kutapika bila kuchukua tahadhari hatimaye kupoteza maisha.

Hivyo Afisa afya huyo aliwatahazalisha wakazi wa manispaa ya Morogoro kuwa makini na ugonjwa huo na kutoa taarifa pindi tu wanapo muona mtu ana dalili za ugonjwa huo ili aweze kupatiwa matibabu haraka Katika eneo husika.

Kwa upande wao baadhi ya wakazi wa kata ya mindu Abed Ibrahim na Chales Ollynkute wamesema kuwa licha ya kuwa ugonjwa huo umeingia Katika manispaa ya Morogoro bado wakazi wake hawana uelewa wa kutosha kuhusiana na kujikinga na ugonjwa huo ambao umekuwa ukipoteza maisha ya watu kutokana na kutokuwa na uelewa wa kutosha.

Kutoka mkoani Shinyanga inaarifiwa kuwa ugonjwa huo umeingia pia na tayari watu watatu wamelazwa katika kambi maalumu iliyofunguliwa leo mchana kwa ajili ya kuwapokea watu wote watakaobainika kuwa na dalili za ugonjwa huo.

Kwa mujibu wa Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dk Mfaume Kibwana wagonjwa hao wamepokelewa leo asubuhi wakiwa na dalili za Kipindupindu.

Dk Kibwana amesema kutokana na wagonjwa hao kuonesha dalili zote za ugonjwa wa Kipindupindu wamelazimika kufungua kambi maalumu eneo jirani na Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Shinyanga ambayo itatumika kuwalaza wagonjwa wote watakaobainika kuugua kipindupindu.

“Mpaka sasa tumepokea wagonjwa watatu leo asubuhi wakiwa wanaharisha na kutapika, tulipowaangalia tunahisi ugonjwa walionao ni Kipindupindu, kwa sasa tumechukua vipimo vyao kwa ajili ya kuvichunguza na taarifa kamili tutaitoa kesho,” alisema Dk Kibwana.
Share on Google Plus

About Aldo Simon

0 comments:

Post a Comment